Proverbs 18


1Mtu ajitengaye na wengine
hufuata matakwa yake mwenyewe;
hupiga vita kila shauri jema.


2 aMpumbavu hafurahii ufahamu,
bali hufurahia kutangaza
maoni yake mwenyewe.


3 Wakati uovu unapokuja, dharau huja pia,
pamoja na aibu huja lawama.


4 bManeno ya kinywa cha mwanadamu ni kina cha maji,
bali chemchemi ya hekima ni kijito kinachobubujika.


5 cSio vizuri kumpendelea mtu mwovu,
au kumnyima haki asiye na hatia.


6 dMidomo ya mpumbavu humletea ugomvi
na kinywa chake hualika kipigo.


7 eKinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake
na midomo yake ni mtego kwa nafsi yake.


8 fManeno ya mchongezi ni kama chakula kitamu;
huingia sehemu za ndani sana za mtu.


9 gMtu aliye mlegevu katika kazi yake
ni ndugu na yule anayeharibu.


10 hJina la Bwana ni ngome imara,
wenye haki huikimbilia na kuwa salama.


11 iMali ya tajiri ni mji wake wenye ngome,
wanaudhania kuwa ukuta usioweza kurukwa.


12 jKabla ya anguko moyo wa mtu hujaa kiburi,
bali unyenyekevu hutangulia heshima.


13 kYeye ajibuye kabla ya kusikiliza,
huo ni upumbavu wake na aibu yake.


14 lRoho ya mtu itastahimili katika ugonjwa
bali roho iliyovunjika ni nani awezaye kuistahimili?


15 mMoyo wa mwenye ufahamu hujipatia maarifa,
masikio ya mwenye hekima huyatafuta maarifa.


16 nZawadi humfungulia njia mtoaji,
nayo humleta mbele ya wakuu.


17 Yeye aliye wa kwanza kuleta mashtaka huonekana sahihi,
hadi mwingine ajitokezapo na kumuuliza maswali.


18 Kupiga kura hukomesha mashindano
na kutenganisha wapinzani wakuu wanaopingana.


19 oNdugu aliyechukizwa ni mgumu kuridhika
kuliko mji uliozungushiwa ngome,
nayo mabishano ni kama malango
ya ngome yenye makomeo.


20 pTumbo la mtu litajaa kutokana na tunda la kinywa chake,
atashibishwa mavuno yanayotokana na midomo yake.


21 qMauti na uzima viko katika uwezo wa ulimi,
nao waupendao watakula matunda yake.


22 rApataye mke apata kitu chema
naye ajipatia kibali kwa Bwana.


23 sMtu maskini huomba kuhurumiwa
bali tajiri hujibu kwa ukali.


24 tMtu mwenye marafiki wengi wanaweza kumharibu,
bali yuko rafiki aambatanaye na mtu kwa karibu kuliko ndugu.
Copyright information for SwhKC